Siku moja baada ya uongozi wa klabu ya Simba kuwaomba mashabiki wake kutowazomea watani wao Yanga katika mchezo wa klabu bingwa barani Afrika dhidi ya St Louis ya Shelisheli kesho hali ni tofauti kwa mabingwa hao.
Kupitia kwa mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Simba Hajji Manara aliwaomba mashabiki wao waache upinzani linapokuja suala la mechi za kimataifa.
Mjumbe wa kamati ya utendaji wa klabu ya Yanga, Salum Mkemi amesema watafurahi kama watani wao watawashangilia lakini wao hawawezi kuthubutu kuwashangilia Wekundu hao.
Mkemi amewaambia waandishi wa habari kuwa itakuwa ngumu kwa upande wao kuwashangilia Simba wanapocheza hata kama ni mechi za kimataifa.
“Kwakweli itakuwa ngumu kwetu kuwashangilia Simba ila wao hatuwakatazi kutushangilia kama wakiamua kufanya hivyo.
“Katika mpira hata kama unataka kuishangilia timu lakini kama haifanyi vizuri itakuwa ngumu kufanya hivyo. Sisi mwaka 1992 tuliishangilia Simba kipindi cha kwanza lakini walipozidiwa uzalendo ukatushinda tukashangilia wageni,” alisema Mkemi.
Pamoja na kauli ya jana ya Manara kuwataka mashabiki wa Simba isiwazomee Yanga lakini itakuwa ngumu kwa Wekundu hao kufanya hivyo.