Kiungo wa klabu ya Arsenal, Henrikh Mkhitaryan hatokua sehemu ya kikosi cha The Gunners leo usiku kwenye mchezo wa Europa League ambao utashuhudia wakicheza ugenini dhidi ya Qarabag ya Azerbaijan.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 ameachwa jijini London nchini Uingereza, kutokana na sababu za kisiasa ambazo zinamzuia kucheza kwenye ardhi ya Azerbaijan.

Mkhitaryan mwenye umri wa miaka 29, amehofia kujumuika na wachezaji wenzake Azerbaijan, kufuatia nchi yake ya Armenia kutokua na mahusiano mazuri ya kidiplomasia na taifa hilo la Ulaya ya Mashariki.

Meneja wa Arsenal Unai Emary amethibitisha kutokuwepo kwa kiungo huyo ambapo amesisitiza kuwa tayari kwa mpambano dhidi ya Qarabag leo usiku.

“Mkhitaryan hakusafiri nasi, ” alisema Unai Emery alipozungumza na waandishi wa habari akiwa Azerbaijan.

“Nina heshimu taratibu zote, ninamheshimu kila mmoja katika timu, nimeheshimu ombi la mchezaji wangu la kutotaka kusafiri nasi, ninaamini anahofia usalama wake,” aliongeza.

“Tumekuja kupambana na tupo tayari kwa hilo, wachezaji wangu wapo tayari na tumejiandaa vilivyo.”

Hii inakua mara ya pili kwa Mkhitaryan kushindwa kusafiri na timu kuelekea Azerbaijan, mara ya kwanza ilitokea alipokua na klabu ya Borussia Dortmund mwaka 2015, walipopangiwa kucheza na Gabala.

Hata hivyo, kuna hatari ya Mkhitaryan kutosafiri kwa mara nyingine na kikosi cha Arsenal kuelekea mjini Baku Azerbaijan, endapo klabu hiyo ya jijini London itafuzu kucheza mchezo wa fainali wa Europa League.

Mchezo wa fainali wa Europa League umepangwa kufanyika mjini Baku, Mei 29/2019, kwenye uwanja wa Olimpiki.

Ebitoke aondoka Timamu TV, afuta kila kitu
Ripoti: Kazi zenye mishahara minono zaidi TZ zatajwa