Serikali imezitaka Wizara na Taasisi kuhakikisha zinaondoa malalamiko ya watumishi kutolipwa mishahara na stahiki zao baada ya kupandishwa madaraja kwa mujibu wa mwongozo wa utumishi wa umma.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais utumishi na utawala bora Kapteni mstaafu George Mkuchika ametoa agizo hilo wakati akifungua mkutano wa baraza kuu la nne la wafanyakazi la utumishi wa umma jijini Dodoma.

Amesema kumekuwa na malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na baadhi ya watumishi kupandishwa madaraja lakini mishahara na stahiki zao kutobadilishwa kwa wakati kulingana na nafasi husika.

“Jambo hili linatakiwa kufanyiwa kazi ondoeni malalamiko ya watumishi kwa kushughulikia madai yao ambayo ni ya msingi mtu amepandishwa daraja lakini mamlaka ipo na haifanyii marekebisho kwa wakati naagiza taasisi na wizara kuondosha haya malalamiko,” ameongeza Mkuchika.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato unaofanywa na watumishi wa umma Waziri Mkuchika amesema anapongeza suala hilo kwani inaonesha ni jinsi gani wapo makini katika kusimamia mapato ambayo yamekuwa yakitumika kuboresha miundombinu mbalimbali.

“Niwapongeze watumishi hao kwa kuwa mstari wa mbele kwenye ukusanyaji na usimamiaji wa mapato hii ni njia nzuri ambayo inasaidia katika kufanikisha uboreshwaji wa mambo mbalimbali kimiundombinu,” amebainisha Waziri Mkuchika.

Hata hivyo mbali na maagizo aliyoyatoa Mkuchika pia amewataka watumishi wa umma walio chini ya ofisi ya Rais utumishi na utawala bora kuhakikisha wanakuwa mfano wa kuigwa katika suala la kupinga rushwa na kuzingatia uadilifu ikiwepo kutochagua maeneo ya kwenda kufanyia kazi.

Awali akiongea katika mkutano huo mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi la utumishi wa umma Leah Ulaya amesema moja kati ya changamoto ambazo zimekuwa kero kwa watumishi ni upandishwaji wa madaraja bila kuzingatia stahiki nyingine ikiwemo mishahara.

Hata hivyo amemshukuru Waziri Mkuchika kwa kuona kilio cha wafangakazi na kuahidi kuwa baraza hilo litafanyia kazi yale yote yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo kwa kuzingatia muda na kwa weledi.

Afya ya Moi yatetereka tena
Kauli ya Jafo uchukuaji wa fomu kwa mbwembwe na shamrashamra