Siku chache baada ya kuthibitishwa hatokuwa kwenye kikosi cha Simba SC msimu ujao 2023/24, Kiungo Jonas Mkude amefunguka mustakabali wake kuelekea dirisha la usajili.
Kiungo aliyedumu kwa miaka 13 ndani ya kikosi cha Simba SC, Juni 23, 2023 alifikia makubaliano ya kuweka pembeni uzi wa klabu hiyo baada ya mkataba wake kugota mwisho na mabosi kumpa mkono wa kwaheri.
Hata hivyo kiungo huyo ameanza kuhusishwa na mpango wa kuwindwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, lakini hadi sasa Uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani haujasema lolote kuhusu tetesi hizo.
Mkude alipoulizwa kuhusu tetesi hizo alijibu kwa kifupi kwa kusema: “Tuombe Mungu.”
Msimu wa 2022/23, Mkude alikuwa shuhuda, Simba SC ikikosa mataji yote waliyokuwa wakipambania ikiwa ni pamoja na Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Azam Sports Federation pamoja na Kombe la Mapinduzi.
Tanzania Prisons wana rekodi zao ikiwa ni timu pekee aliyoitungua bao moja kwenye Ligi Kuu Bara 2022/23 kati ya mabao 75 yalifungwa na timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira raia wa Brazil.
Mkude katika maisha yake ya soka la ushindani, amecheza Simba SC kwa misimu 11, huku misimu miwili akicheza Simba SC U20. Pia ameitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.