Kiungo wa Simba, Jonas Mkude atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili baada ya kuumia vidole vya mguu wa kulia mwanzoni mwa juma lililopita.
Kwa muda huo ambao Mkude atakuwa nje, ataikosa michezo minne ya Ligi Kuu ambayo Simba itacheza dhidi ya timu za Ruvu Shooting, Mwadui FC, Prisons na Mbeya City na ikiwa atapona na kuwa fiti kwa wakati, anaweza kuonekana uwanjani katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Azam FC utakaochezwa Julai Mosi jijini.
Mkude aliumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC uliofanyika kwenye uwanja wa Mo Simba, Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam baada ya kukanyagana na beki, Kelvin Kijili.
Taarifa iliyotolewa na klabu ya Simba inasema Mkude ataendelea na mazoezi mepesi pamoja na matibabu akiwa nje ya uwanja.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema wanaendelea kumpa matibabu kiungo huyo ili ndani ya wiki mbili awe ameimarika na kuendelea na mazoezi.
“Mkude yuko katika uangalizi maalumu wa matibabu yake ili baada ya hizo wiki mbili awe ameimarika na kurejea kuendelea na mazoezi,” alisema Dk Gembe.
Mkude alikanyangana na Kijili wakiwa katika harakati za kuwania mpira, ambapo Kijili alisema aliudokoa mpira huo na Mkude akapiga vidole chini ya meno ya viatu.
“Nia ilikuwa tuchukue mpira, mimi nikamuwahi, sikumchezea rafu, niliubetua mpira bahati mbaya yeye akaingiza mguu kwenye meno, akapata shida kwenye vidole,” alikaririwa Kijili hivi karibuni.
Katika mchezo huo, Mwamuzi Said Pambalelo alisimamisha mpira ili kuruhusu Mkude apewe huduma ya kwanza kabla ya madaktari wa Simba kumtoa nje na kuendelea kumpa huduma ya kwanza kisha wakaita gari la wagonjwa lililompeleka hospitali.
Hata hivyo kutokana na idadi kubwa ya viungo ilionao, Simba huenda isiathirike sana na kukosekana kwa Mkude katika mechi hizo nne kwani pengo lake linaweza kuzibwa ama na Mzamiru Yassin, Said Ndemla au Gerson Fraga lakini pia hata Erasto Nyoni na Shomary Kapombe wanamudu kucheza nafasi yake.