Nyota watatu wa Young Africans wamerejea kikosini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuivaa Azam FC, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu unaotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Oktoba 25.
Metacha Mnata, Farid Mussa na Jonas Mkude hawakuhusika kwenye mechi tatu zilizopita kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matatizo ya kifamilia na utovu wa nidhamu, lakini sasa wameitwa kambini kujiandaa na mechi zijazo.
Metacha na Mkude walidaiwa kusimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu, huku Farid akiwa na ruhusa maalumu na kukosa mechi ya marudiano dhidi ya Al Merreikh, Ihefu FC na Geita Gold.
Kocha wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema kuwa atatumia kipindi hiki cha mapumziko kuboresha kikosi chake na kuleta usawa.
“Ni muda wa mapumziko, baadhi ya wachezaji wetu wamekwenda kujiunga na timu zao za Taifa.
“Tutaendelea na mazoezi na hawa waliopo na lengo ni kuboresha na kuweka usawa wa kikosi chetu,” amesema Gamondi aliyeifikisha Young Africans hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25 ikisota bila kufika hatua hiyo.