Wachezaji Jonas Mkude na Israel Mwenda wapo tayari kwa mpambano wa Mzunguuko wa tatu wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Simba SC itakua mgeni katika mchezo huo mjini Casablanca nchini Moroco Jumapili (Februari 27), huku wachezaji hao wakipona majeraha yaliyosababisha kukosa mchezo wa Mzunguuko wa Pili dhidi ya USGN ya Niger ulioisha kwa sare ya 1-1.
Wachezaji hao waliugua ghafla baada ya kuwasili mjini Nieamy Jumamosi (Februari 19).
Daktari wa Simba, Edwin Kagabo amesema Mkude na Mwenda wameungana na wenzao katika maandalizi ya mchezo dhidi ya RS Berkane, baada ya kuwasili mjini Casablanca jana Jumatano (Februari 23).
“Mkude na Mwenda wote wapo sawa kiafya tofauti na ilivyokuwa siku moja kabla ya kucheza na USGN, kuhusu kama watatumika kwenye mchezo wetu dhidi ya RS Berkane hilo ni la suala la Benchi la Ufundi.” amesema Kigabo.
Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ kwa kufikisha alama 04, ikifuatiwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 03 sawa na RS Berkane huku USGN ikiburuza mkia kwa kuwa na alama moja.