Kiungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Jonas Mkude, amefurahia kuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi nyingi zilizowakutanisha watani wa jadi Simba SC na Young Africans.
Pia, nyota huyo amesema hatua hiyo imemfanya ajivunie na kujiona ni mchezaji mkubwa nchini.
Kiungo huyo wa kati, alitua Young Africans katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu, akitokea Simba SC alipodumu kwa miaka 13.
Kwa mujibu wa kiungo huyo maarufu kama ‘Nungunungu’, dabi ya mwishoni mwa juma lililopita ambayo Young Africans ilishinda mabao 5-1, ilikuwa ya 30 kwa upande wake kucheza. “Hii ilikuwa dabi yangu ya 30,” amesema kiungo huyo.
Mkude ameongeza kuwa: “Katika dabi hizo (30), mara nyingi Simba SC ilikuwa inashinda na huu ndio mchezo wangu wa pili nikiwa Young Africans,”.
Akizungumzia dabi iliyopita, Mkude amesema amefurahishwa na kikosi chao kuibuka na ushindi wa mabao 5-1.
“Nina furaha timu yangu kupata ushindi kwa sababu (Simba SC) ni katika timu ya Ligi Kuu tuliyokuwa tukiihofia,” amesema.
Nyota huyo ametaja timu ambazo awali Young Africans ilikuwa ikizihofia ni Singida Fountain Gate, Azam FC na Simba ambazo hivi sasa zote wamezifunga.