Kiungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Jonas Mkude ameweka wazi kuwa licha ya kushinda mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba SC, ni mapema sana kusema tayari wameshaingia katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Mkude amesema anaamini kwa kujiandaa na kutafuta pointi tatu muhimu katika kila mechi ambayo iko mbele yao ndicho kitu pekee kitakachowawezesha kufikia malengo yanayotarajiwa na Wanachama na Mashabiki wa Young Africans.
Amesema kitendo cha kumfunga Simba SC hakina maana kuwa wamemaliza kila kitu na kujihakikishia ubingwa kwa sababu ligi bado ni ndefu na wana michezo zaidi ya 20 ambayo hawajacheza.
“Ushindi wa Simba SC unatuweka katika nafasi nzuri za kujihakikishia tunaendelea kusalia kileleni, suala la ubingwa ni mapema sana tunatakiwa kushinda na kutafuta matokeo chanya kila mechi ili kufikia malengo yetu na yanayotarajiwa na wanayanga.
Ligi imekuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kujiandaa vizuri, tumeshinda mechi kubwa lakini unaweza kupoteza mechi ndogo, tunaamini katika kujiandaa,” amesema kiungo huyo.
Ameongeza kuwa anaimani kubwa ya kufanya vizuri kwenye ligi kulingana na kila mchezaji ndani ya Young Africans malengo yake ni kuhakikisha wanapambana kutafuta matokeo ili kutetea ubingwa msimu huu 2023/24.