Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Katavi kuwachunguza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira Mpanda (MUWASA), Hussein Nyemba kwa tuhuma za kukiuka taratibu za manunuzi ya ummana Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Abraham Casto anayedaiwa kujipatia ardhi katika vijiji mbalimbali bila kufuata taratibu za kisheria.
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majliwa wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri za Mpanda, Nsimbo na Tanganyika wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Katavi huku Watumishi wote wawili wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Amesema, TAKUKURU pia inatakiwa kuchunguza ununuzi wa pikipiki 30 zenye gharama ya shilingi. milioni 3.8 kila moja huku Wilayani Mpanda pikipiki moja ikiuzwa shilingi. milioni 2.7, ununuzi wa mita za maji 1,000 uliofanywa bila ya kukaguliwa na TBS pamoja na ajira za watumishi 25 zilizofanywa bila kibali.
Majaliwa ameongeza kuwa, “Rais amesema hatomvumilia mtumishi yeyote ahakikishe anasimamia majukumu yake. Watumikieni wananchi bila ya kuwabagua, sisi ni wahudumu wa wananchi lazima tufanye kazi na pangeni muda wa kuwafuata katika maeneo yao na kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi”
Aidha, ametumia fursa hiyo kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi ahakikishe Idara ya Ardhi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilayani inasimamiwa vizuri na kusema, “Idara ya ardhi mkoa ijitathmini migogoro ni mingi na haishughulikiwi ipasavyo. Wananchi wana migogoro mingi ya ardhi.”
Agizo hilo ni utekelezaji wa maagizo Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Omari Kinana aliyoyatoa alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Katavi tarehe 25 Julai, 2022. Miongoni mwa maagizo aliyoyatoa ni pamoja na kuitaka idara ya ardhi mkoa wa Katavi itazamwe kutokana na kugubikwa na rushwa na ujanja ujanja.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa Idara katika Halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani waibue vyanzo vipya vya mapato na wahakikishe wanafahamu kiasi cha fedha kinachokusanywa katika kila eneo badala ya kuweka makadirio.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa muda wa mwezi mmoja kwa watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika ambao wanaishi katika Halmashauri ya wilaya ya Mpanda wakiwemo baadhi ya wakuu wa Idara wawe wamehamia Tanganyika ifikapo Januari 15, 2023 ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Haya hivyo, Waziri Mkuu pia ameagiza mkataba wa mradi wa kuzalisha hewa ukaa ambao unahusisha misitu ya vijiji vinane yenye ukubwa wa hekta 216,944 za ardhi na wakazi 34, 242 katika wilaya ya Tanganyika ukafanyiwe uchunguzi kwa mwanasheria ikiwa ni pamoja na kupitia masharti yaliyowekwa.