Aliyekuwa Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Dkt John Pima na wenzake wawili wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 kila mmoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi, yaliyokuwa yakiwakabili.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Saraphina Nsana katika kesi namba 5 ya mwaka 2022 ya uhujumu uchumi ambapo wengine waliohukumiwa ni Mariam Mshana aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji, na Innosenti Maduhu.
Awali akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nsana alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imejidhisha pasi na shaka kwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka hivyo kuwatia hatiani wahusika hao.
“Kwa kuzingatia ushahidi huo na kwamba kama washtakiwa wanarekodi ya makosa ya jinai ,na utegemezi wa familia mahakama inawahukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja na iwapo kama hamjaridhika na adhabu hiyo nafasi ya kukata rufaa ipo wazi,” alisema Hakimu Nsana.