Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ametoa siku saba hadi kufikia tarehe 21 Mwezi huu kuanzia leo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Emanuel Jonson kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mwaweja kata ya Negezi Wilaya ya Kishapu ili wananchi waanze kupata matibabu kijijini hapo.
RC Sengati ametoa agizo hilo baada ya kutembelea ujenzi wa zahanati hiyo nakugundua mapungufu yaliyopo na hivyo kutoa muda wa wiki moja kwa mkurugenzi huyo ili kuwezesha kituo hicho kuanza kutoa huduma kwa kuwa ujenzi huo umechukua muda mrefu bila kukamilika licha ya uwepo wa fedha.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile ameitaka Halmashauri ya Kishapu kukamilisha Zahanati hiyo ili kituo hicho kisajiliwe na kuingizwa katika orodha ya kupatiwa dawa.
Hata hivyo Furaha ya wakazi hao inakuja kufuatia ziara ya Mkuu wa Mkoa kufika kituoni hapo kujionea marekebisho ya ujenzi wa Zahanati hiyo ambapo awali Kamati ya Siasa ya Mkoa ilifika katika zahanati hiyo na kushauri kufanyika marekebisho kwa kipindi cha mwezi mmoja.