Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (Taliri), Kanda ya Kati, Dkt. Harun Chawala na mkewe Neema Mwasanganga waliofariki dunia usiku wa juzi baada ya gari lao kusombwa maji wakati wakivuka daraja la Shaaban Robert mjini Mpwapwa wanaagwa leo.

Akizungumza leo Jumapili Machi 7, 2021 Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Archard Rwezaura amesema kuwa miili ya wanandoa hao inaagwa leo nyumbani kwao Taliri wilayani humo.

“Sasa hivi ndio tunakwenda kuaga miili halafu itasafirishwa kwenda nyumbani kwa mwanaume (Dk Chawala) Wilayani Kilolo mkoani Iringa,”amesema Dkt Rwezaura.

Amesema mazishi ya wanandoa hao yatafanyika kesho nyumbani kwa Dkt. Chawala Wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Dkt. Jonas Kizima, Chawala alikuwa anampeleka mkewe kazini katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa lakini walipofika kwenye daraja la Shaban Robert maji yaliwazidi na kusombwa.

Tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku kwa gari lao aina ya Nissan X-trae yenye usajili namba T483 BRR kusombwa na maji kwenye daraja hilo lililopo mita chache kutoka ilipo ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Kutoka gari ilipotumbukia hadi ilikokutwa miili ni umbali wa karibu kilomita 18 na ilikuwa katika maeneo tofauti .

Mashuhuda wanasema mwili wa mwanamke ulikutwa Kitongoji cha Kwamshango ambako ni kilomita 15 kutoka walipotumbukia wakati mwili wa Dkt. Chawala ulikutwa Kitongoji cha Isinghu ambako ni kilomita 18.

Mahali ulipokutwa mwili wa Dkt. Chawala ilikuwa ni mpakani mwa Isinghu na Gulwe ambako unapita mto mkubwa wa Kinyasungwi unaounganisha na bwawa kubwa la Kidete mkoani Morogoro.

Mwinyi apatia ufumbuzi Kiwanda cha Sukari
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 7, 2021

Comments

comments