Boeing imemfuta kazi mkurugenzi mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, Dennis Muilenburg, katika hatua ya kurejesha imani ya kampuni hiyo baada ya ajali mbili mbaya zilizohusisha ndege yake ya 737 Max.
Boeing imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la uchunguzi mkali dhidi ya ndege za 737 Max kufuatia ajali zake zilizotokea katika kipindi cha miezi mitano, ya kwanza ikiwa ni ya Indonesia na baadaye ya Ethjiopia.
Safari za ndege za za 737 zimepigwa marufuku kusafiri kote duniani tangu mwezi Machi, wiki iliyopita Boeing ilisema kuwa itasitisha uzalishaji wa ndege zake.
Huku kampuni hiyo ikiwa na matumaini ya kurejesha angani ndege zake ambazo ndizo zinazouzwa zaidi duniani kufikia mwishoni mwa mwaka huu , wakaguzi wa viwango vya ndege nchini Marekani wamesema wazi kuwa haitapata kibali cha kurejea angani haraka.
Bodi ya Boeing ilisema “imeamua kuwa mabadiliko ya uongozi wake ni muhimu ili kurejesha imani katika kampuni inapojaribu kusafisha uhusiano wake na wasimamizi wa viwango vya safari za anga, wateja na wadau wote “.
Bwana Calhoun, mkurugenzi mtendaji wa masuala ya usalawa, atachukua wadhfa wake kuanzia Januari 13.