Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,  Profsa Joyce Ndalichako amemfutia mkataba Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya elimu ya Juu (HESLB), George Nyatage pamoja na wakurugenzi wengine watatu wa Bodi hiyo kutokana na kushindwa kusimamia Bodi hiyo na kupelekea upotevu wa kiasi kikubwa cha fedha.

Mkurugenzi Bodi ya Mikopo

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua hiyo aliyoichukua, Profesa Ndalichako amesema kuwa Bodi hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo na kwamba hulazimika kufanya maandamano ili wapate mikopo hiyo wakati ni makosa na uzembe wa watu wachache.

Watumishi wengine waliokutana na panga hilo, ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Juma Chagonja pamoja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer. Watumishi hao wamesimamishwa kazi.

Profesa Ndalichapo amesema kuwa Serikali imebaini upotevu wa fedha za umma unaotokana na Bodi hiyo kuwalipa baadhi ya wanafunzi mikopo mara mbili au kuelekeza kiasi kikubwa cha mikopo hiyo sehemu isiyostahili.

Alieleza kuwa kutowajibika ipasavyo kwa watendaji hao, kumelekea wanafuzi 23 kupewa mikopo katika vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu mfululizo. Alisema katika chuo cha kwanza, Bodi hiyo iliwalipa wanafunzi hao kiasi cha shilingi shilingi milioni 653 na katika chuo cha pili iliwalipia zaidi ya shilingi milioni 147.

Kadhalika, Profesa Ndalichako amesema kuwa kumbukumbu zinaonesha kuwa wanafunzi 169 walipewa mikopo na Bodi hiyo katika vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu mfululizo. Chuo cha kwanza kililipwa shilingi milioni 658 na chuo cha pili shilingi milioni 665. Mbali na hilo, Bodi hiyo iliendelea kuwalipa kiasi cha shilingi milioni 136 wanafunzi wanafunzi 55 walioacha masomo na shilingi milioni 342 zililipwa kwa wanafunzi wa vyuo wasiokuwa na usajili katika vyuo husika.

Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa Bodi hiyo iliendelea kuwalipa wanafunzi waliokwenda masomoni Algeria wakati mkataba wao wa kupewa mikopo ulikwisha miaka 7 iliyopita.

Aliongeza kuwa kaguzi zimebaini zaidi ya shilingi milioni 159 zililipwa kwa wanafunzi 306 kwa zaidi ya kiwango kilichobainishwa kutokana na muongozo wa upangaji wa maraja ya mikopo wa mwaka 2009/2010.

 

Mandawa Afuata Nyayo Za Mbwana Samatta
Katiba Mpya; NEC yatangaza kuanza mchakato wa kura ya maoni