Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakurugenzi wa Mashirika ya umma kujiandaa kisaikolojia, akisema kuwa shirika lolote litakalo kufa, litaondoka na nafasi ya Mkurugenzi wake.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Agosti 19, 2023 wakati alipokuwa akifungua Kikao Kazi Cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kinachofanyika leo katika Ukumbi wa AICC uliopo jijini Arusha.
“Ujumbe kwa M-CEO wa Mashirika ya Umma, shirika likifa, nawe utalazimika kupoteza nafasi yako kwa sababu mkakati tuliokuwa nao kama Taifa ni kufanikisha dira na maendeleo kwa kupitia nyanja mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma ambayo leo tumekuja hapa kujadili ufanisi wake.
Shirika likifa kufa nalo,” alisema Rais Samia. Katika kikao kazi hicho, pamoja na mambo mengine, Rais Samia alipata nafasi ya kutoa dira na taswira nzuri ya kuyapatia mafanikio mashirika hayo, ambayo yatahusisha Wananchi kwa kununua hisa zake, ili wawe na sauti katika uendeshaji wake.