Taharuki imetanda nchini Kenya baada ya Kaimu Mkurugenzi wa teknolojia wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (IEBC), Christopher Musando aliyepotea hivi karibuni kupatikana akiwa amefariki katika eneo la Kikuyu jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa vyombo vya usalama nchini humo, Musando alifanya mawasiliano ya mwisho Jumamosi majira ya saa tisa alfajiri ambapo alituma ujumbe mfupi kwa mmoja kati ya wafanyakazi wake.
Jeshi la polisi nchini humo limesema kuwa mwili wa Musando ulipatikana pamoja na mwili wa mwanamke mwingine ambaye hakutambulika mapema na kisha kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti jijini humo.
Marehemu alikuwa na jukumu la kusambaza vifaa vya kielektroniki ambavyo vitatumika kuwatambua wapiga kura na kusambaza matokeo ya uchaguzi mkuu kutoka katika vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa vyombo vya usalama kuhusu upelelezi wa tukio hilo na yaliyomkuta Musando.
Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu, uchaguzi unaotajwa kuwa wa ushindani zaidi katika historia ya nchi hiyo.