Mkurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ladslaus Matindi amesema kuwa ndege aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa katika matengenezo imeanza kufanya safari zake kama kawaida.
Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Power BreakFast cha CloudsFm akizungumzia kuhusu taarifa ambazo zimesambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha ndege hiyo ikiwa katika matengenezo.
Amesema kuwa ndege hiyo ilikuwa na hitilafu na ilitengenezwa kwa siku moja na tayari imerejea katika ratiba ya safari zake za kila siku.
”Ndege inaweza kuharibika, kupata hitilafu, au kuingiliwa na kitu chochote kutoka nje kwakuwa ni mashine hakuna namna ya kuzuia, hilo ni jambo la kawaida hata katika mwili wa binadamu,”amesema Matindi
Aidha, Matindi ameongeza kuwa ndege hiyo ipo Dar es salaam na matengenezo yake yamechukua siku moja, ambapo amebainisha kuwa matengenezo yalianza jumatatu mchana hadi jana mchana.
”Ndege zinazoharibika sio za ATCL pekee bali popote hata KLM Ndege zao huwa zinaharibika, British Airways na Emirates wakisema ndege zao hazijawahi kuharibika hapo ndipo tujiulize kwanini zetu zinaharibika,”amesema Matindi