Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu nchini Kenya, Dennis Itumbi amekamatwa na polisi kwaajili ya mahojiano kuhusu barua ya njama ya kutaka kumuua naibu rais, William Ruto.
Itumbi amekamatwa na wapelelezi wanaochunguza tuhuma za njama hizo za kutaka kumuua naibu rais William Ruto.
Denis Itumbi anashikiliwa makao makuu ya Idara ya Upelelezi jijini Nairobi nchini humo na amekamatwa siku chache zilizopita baada ya taarifa kwamba chanzo cha barua hiyo ya kughushi imetambulika kuwa ilipitia mikononi mwake.
Aidha, wiki iliyopita, mawaziri kadhaa nchini Kenya walikana kupanga njama za kutaka kumuua Naibu rais nchini Kenya, William Ruto.
Waziri wa biashara wa nchi hiyo, Peter Munya amekana tuhuma za kupanga mauaji ya Naibu Rais, William Ruto wakati akizungumza nje ya Makao Makuu ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambako aliitwa sambamba na mawaziri wengine kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.
Gazeti la The Standard limeripoti kuwa mawaziri hao wanatuhumiwa kufanya vikao vya siri, lakini Munya amewaambia waandishi wa habari kuwa hawajapeleka taarifa polisi kwa kuwa, William Ruto hajapeleka malalamiko rasmi.
Kwa upande wa Gazeti la Daily Nation la Kenya limemnukuu waziri huyo akisema kuwa Naibu Rais William Ruto alidai kuwa mawaziri hao walikuwa wakifanya vikao vya siri na maafisa wengine.
Hata hivyo, Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ana mipango ya kugombea kiti cha urais mwaka 2022 kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.