Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Ally Mayay amezishauri Simba SC na Young Africans kuelekea michezo ya Hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Young Africans ilitinga hatua hiyo kwa kuwabanjua Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC jumla ya Mabao 9-0, huku Simba SC ikiwatoa Mabingwa wa Malawi Nyasa Big Bullet kwa ushindi wa jumla wa 4-0.
Katika hatua hiyo Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kwa kuwakabili Mabingwa wa Sudan Al Hilal, huku Simba SC ikipangiwa kuanza ugenini dhidi ya Primira de Agosto ya Angola kati ya Oktoba 07-09.
Ally Mayay ambaye jana Jumanne (Septemba 20) alitangazwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo iliyokua inashikwa na Yusuph Omar Singo, amezitaka timu hizo Kongwe nchini kuhakikisha zinajipanga vizuri, ili kufikia lengo la kusonga mbele kwenye Michuano hiyo ya Afrika.
Hata hivyo Mayay amesema Young Africans ndio yenye mlima mrefu wa kupanda tofauti na ndugu zao Simba SC, kutokana na mazingira ya mchezo wao dhidi ya Al Hilal yalivyokaa.
“Simba SC ina nafasi nzuri ya kutinga hatua ya Makundi kwa sababu wanaanzia ugenini na kumalizia nyumbani, lakini Young Africans wataanzia nyumbani na kumaliza ugenini, tena kwa timu ngumu na yenye uzoefu mkubwa katika Michuano hii.
“Young Africans wanachotakia ni kupata ushindi mkubwa katika mchezo wa nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri watakapokwenda ugenini nchini Sudan, kinyume na hapo hali itakua ngumu sana kwao.”
“Lakini yote kwa yote timu zote hizi, zinapaswa kujipanga na kujiandaa vizuri ili kupambana katika michezo yao hii ya Kimataifa, sisi Watanzania wote tunazitazama kama wawakilishi wetu na watetezi wetu kimataifa” amesema Mayay
Ikiwa Young Africans na Simba SC zitafuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, zitajihakikishia kitita cha fedha kiasi cha Dola za Marekani 550,000 sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 1.3 kila mmoja, kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Na kama itatokea Young Africans na Simba SC zikatolewa katika hatua hiyo, zitaangukia hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, endapo zitafuzu hatua ya Makundi zitajihakikishia Dola za Marekani 275,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 641kila mmoja, kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.