Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt Athuman Kihamia amempa siku saba Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kumuomba radhi kutokana na kauli na kejeli alizozitoa dhidi yake.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa marudio katika majimbo ya Ukonga na Monduli na Kata 23.
Amesema kuwa Mbowe akiwa katika mkutano na wanahabari alitoa shutma kwa NEC huku shutma nyingine zikimlenga yeye Dkt. Kihamia moja kwa moja.
Aidha, amesema kuwa katika mkutano huo Mbowe alisema wakurugenzi wa halmashauri ni makada wa CCM huku polisi wakitumika na mkurugenzi wa uchaguzi anaujua mchakato huo lakini amekaa kimya.
“Namwambia (Freeman) Mbowe achague maneno ya kuongea yeye ni kiongozi mkubwa wa chama, achuje maneno yake na awe na ushahidi, mimi sipendi kulumbana na wanasiasa na asitafute kiki,” amesema.
Hata hivyo, Dkt. Kihamia ameongeza kuwa Mbowe asipoomba radhi basi Watanzania wawe makini kutokana na kauli zake.