Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yupo jijini Rome, Italia ambapo atamuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani litakalofanyika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo – FAO, Oktoba 16-20, 2023.

Mkutano huo wa Wakuu wa nchi na Serikali, utaambatana na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani pamoja na maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo -FAO.

Aidha, jukwaa hilo pia linatarajiwa kuwakutanisha wadau wa kilimo wakiwemo Vijana, Wakulima, Wazalishaji wadogo, Watunga sera, Wawekezaji katika Kilimo na Wanasayansi duniani, wakilenga kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula, ili kufikia mustakabali bora wa chakula kwa wote bila kumwacha mtu nyuma.

Jukwaa hilo pia litaweka msisitizo kwa nchi husika katika kuchukua hatua za ndani zinazojikita kwenye uvumbuzi, ushirikiano, sayansi, ushirikishwaji wa Vijana, wazawa, Wanawake na watu walio katika Mazingira magumu.

Siku nne, Wakuu wa nchi na Serikali kutoka nchi shiriki 31 watapata fursa ya kushiriki katika Mpango wa “Hand-in-Hand Initiative,” ambapo watawasilisha mipango ya uwekezaji iliyopewa kipaumbele nchini mwao na kuonesha fursa kwenye maeneo ambayo Mpango huo wa Shirika la Chakula na Kilimo unasaidia Serikali kupunguza umaskini na njaa.

Viongozi Wakuu watakaohudhuria ni Rais wa Italia, Sergio Mattarella, Rais wa Ireland, Michael Higgine, Mfalme wa Lesotho, Viongozi wa Ujumbe kutoka Nchi Wanachama na Viongozi Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (FAO, IFAD & WFP).

Umeme Vijijini: Bado Vijiji sita - Kapinga
Jose Miquissone anarudi mdogo mdogo