Tanzania imepokea na kupongeza azimio la kuanzishwa kwa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na kusisitiza kuwezesha utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa Kuhifadhi Bioanuai kupitia Mikakati ya Kitaifa ya Kuhifadhi Bionuai.
Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia – GEF, unaofanyika Vancouver nchini Canada na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga wakati akiongoza Ujumbe wa Tanzania.
Pamoja na kuzipongeza nchi zilizotoa ahadi ya kuchangia Mfuko huo, Tanzania pia imeziomba nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuwezesha ukusanyaji wa fedha za kutosha katika Mfuko husika.
Mfuko wa Mazingira wa Dunia ni moja ya Mifuko wa Kimataifa inayowezesha shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani hususan katika nchi zinazoendelea.
Shughuli zinazowezeshwa ni pamoja na Hifadhi ya Bioanuai, Mabadiliko ya Tabianchi, Matumizi bora ya Ardhi, Udhibiti wa Taka hatarishi na Kemikali pamoja na Hifadhi ya maji yanayovuka mipaka.