Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umefanyika leo jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (video conferencing) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) .
Mkutano huo umefunguliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Maafisa Waandamizi/ Makatibu Wakuu, Balozi, Wilbert Ibuge ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wajumbe wengine ni waliohudhuria ni Katibu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utaii Dkt. Aloyce Nzuki pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipago, Amina K. Shaaban.
Pamoja na mambo mengine, Kikao hicho kimejadili masuala mbalimbali ndani ya Jumuiya ikiwemo mlipuko wa Virusi vya Corona ndani ya SADC.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri utafanyika Mei 29, 2020 baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa Waandamizi/Makatibu Wakuu.
Mkutano huo utaangalia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Aprili 2020 kuhusu mlipuko wa virusi hivyo na athari zake katika utekelezaji wa programu za SADC, kijamii, kiuchumi ndani ya Jumuiya.
Aidha, Mkutano huu pia umejadili Hali ya kifedha ndani ya Jumuiya, utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC ambayo ni Menejimenti ya Maafa, utekelezaji wa kaulimbiu ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC isemayo ‘Mazingira Wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC’; na mapitio ya hali halisi ya biashara baina ya nchi, maendeleo ya viwanda ndani ya Jumuiya na taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa Jumuiya na mpango kazi wake.
Mkutano huo umehusisha wataalamu kutoka nchi wanachama 12 wa jumuiya hiyo kutoka sekta za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha na Mipango, Uchukuzi na Mawasiliano, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii pamoja na Afya.
Nchi zilizoshiriki Mkutano huo ni Angola, Afrika Kusini, Comoro, Eswatini, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.