Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC umeanza hii leo Lilongwe nchini Malawi ambapo taarifa kuhusu hatua ya kutafsiri nyaraka za kisheria na sera za Jumuiya katika lugha ya Kiswahili pamoja na ujenzi wa sanamu ya Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere yatajadiliwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mwezi Agosti,2021 uliidhinisha kiasi cha Dola za Kimarekani 73 elfu nukta 5 kwa ajili ya kutafsiri nyaraka za kisheria na sera za SADC kwa lugha ya Kiswahili pamoja na kutaja ajenda nyingine zitakazojadiliwa.
Kuhusu ujenzi wa sanamu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere itakayowekwa katika kituo cha Amani na Usalama cha Umoja wa Afrika Addis Ababa nchini Ethiopia Balozi Sokoine ameitaja kampuni ya Epitome Architects ya Dodoma, Tanzania ndio iliyoshinda zabuni hiyo na kwamba uzinduzi wa ujenzi wa sanamu hiyo utakuwa ni sehemu za maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa.
Balozi Sokoine ameyataja masuala mengine yatakayojadiliwa ambayo yana umuhimu mkubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni suala la ajira za watumishi katika kituo cha kanda cha kupambana na ugaidi pia nafasi za ajira za Naibu Katibu Mtendaji wa masuala ya utawala wa SADC.
Pia masuala ya matokeo yatokanayo na mkataba mpya wa ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya nan chi za Afrika,Pasifiki na Caribbean (OACPS) na programu ya ujirani,maendeleo na ushirikiano wa Kimataifa yatajadiliwa.
Mkutano huo unahudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi Amina Shaaban, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Exavier Daudi pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt.Evaristo Longopa.