Waziri wa Nishati na Madini wa Jamhuri ya Burundi Ibrahim Uwizeye amefika nchini kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini hususan utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nikeli.

Ziara ya Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi nchini inakuja baada ya kuhudhuria mkutano wa madini ambao ulikuwa wa manufaa kwa nchi hiyo, ambapo amemuomba Waziri wa Madini Dkt Dotto Biteko kuja kujifunza zaidi kutoka kwa Tanzania kutokana na namna ilivyofanikiwa katika usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya madini ili hatimaye rasilimali madini zinazopatikana nchini Burundi zilinufaishe taifa hilo.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Waziri wa Madini Dkt. Biteko amesema imelenga kujifunza kupitia mradi huo ili kuona namna ambavyo nchi hiyo inaweza kujifunza kutoka Tanzania na namna ambavyo nchi hizo zinavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya namna hiyo.

“Mradi wa Kabanga Nikeli na Msongati nchini Burundi ni mmoja, jiolojia ya Kabanga na Msongati ni moja na kama mnavyojua jiolojia haina mipaka isipokuwa mipaka ya kiutawala. Pia, wamefika kuona namna nchi hizi zinavyoweza kufanya ili hatimaye ziweze kuwa mfano bora wa ushirikiano kwa mataifa mengine Afrika,” amesema.

Aidha, Waziri Biteko ameonya wale wote wanaotegesha kwa lengo la kunufaika na malipo ya fidia na kueleza kuwa hawatalipwa chochote isipokuwa tu kwa wananchi wenye uhalali wa kulipwa, na Serikali haitawavumilia wale wote wanaofanya vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Waziri Uwizeye amesema ujumbe wake umefika nchini kujifunza ili mradi huo uweze kuzinufaisha nchi zote ikiwemo kuhakikisha nchi hiyo pia inachimba madini hayo na hivyo kuiomba Tanzania kuipa nafasi ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa jiolojia ya madini hayo pia inapatikana nchini humo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi amemhakikishia Waziri Biteko kuwa, Wilaya hiyo haitokuwa kikwazo cha utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa nikeli.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo pia kumuomba Waziri Biteko kuweka msukumo ili kuwezesha mradi huo kuanza kwa wakati uliopangwa.

Akizungumza katika ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Gilly Maleko amesema baada ya kuwepo mahusiano mazuri ya kidiplomasia kwa nchi hizo ambazo zimekuwa marafiki kwa miongo mingi, ilionekana kuwa ipo haja ya kukuza mahusiano ya kiuchumi.

Naye, Balozi wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania, Gervouis Abayeho, amesema baada ya kufahamu kuwa Tanzania ina uzoefu wa muda mrefu katika Sekta ya Madini, nchi hiyo imeona ipo haja ya kujifunza kutoka Tanzania ili kupata uzoefu utakaoiwezesha nchi hiyo kusimamia Sekta ya Madini kwa manufaa ya nchi hiyo ikiwemo kuzisaidia nchi hizo kugeuza sura za kiuchumi kwa mataifa hayo.

Kadhalika, Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro, ameihakikishia nchi hiyo kuwa kama mbunge wa eneo hilo atahakikisha anapambania ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara na umeme ili utekelezaji wa mradi huo ufanyike kikamilifu.

Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nikeli Benedict Busunzu akiwasilisha taarifa kuhusu mradi huo amesema uhai wa mgodi unatarajiwa kuwa zaidi ya miaka 30 na kuongeza kuwa, tayari Kampuni hiyo imepata mbia mwenza Kampuni ya BHP ambayo ni kampuni kubwa ya madini duniani inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia katika utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumzia soko la madini hayo duniani, amesema ni yanahitajika sana kutokana na kuhama kwa matumizi ya teknolojia na kueleza kuwa, kabla ya kuzuka kwa vita ya Urusi na Ukraine bei ya madini hayo kwa tani ilikuwa ni Dola za Marekani 21,000 na kupanda hadi Dola za Marekani 51,000 na ndani ya muda mfupi kufikia Dola za Marekani 100,000 kwa tani moja ya nikeli. Ameongeza kuwa, hivi sasa bei yake imeshushwa hadi kufikia Dola za Marekani 48,000 kwa tani ili kulinda mwenendo wa soko

Nitanzungumza na Polepole kwa Kirefu-Rais Samia
RS Berkane wathibitisha kutuma barua CAF