Tanzania inashiriki Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofunguliwa Agosti 8, 2023 jijini Luanda, nchini Angola kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi.
Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, imeeleza kuwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC, imeshuhudiwa ikikabidhi uenyekiti wa ngazi hiyo kwa Angola ambayo itashikilia wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja, hadi Agosti 2024.
Tanzania ambayo ni moja ya nchi waasisi wa SADC, inashiriki kikamilifu Mkutano huo na kwa ngazi ya maafisa waandamizi, na ujumbe wake unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Shaban.
Wakati wa makabidhiano ya uenyekiti, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Kikanda wa DRC, Balozi Songhu Kayumba alisema, kwa mwaka mmoja wa uenyekiti wa DRC, nchi wanachama ziliunganisha nguvu kuhakikiasha kuwa wanafikia malengo waliyojiwekea.
Malengo hayo, yaliongozwa kupitia kaulimbiu isemeyo “Kuhamasisha Uwekezaji katika viwanda kupitia usindikaji wa mazao ya kilimo, madini, kuendeleza mnyororo wa thamani wa kikanda kwa nia ya kufikia uakuaji wa uchumi jumuishi na endelevu” (Promoting Industrialization through Agro-Processing, beneficiation of minerals and the development of regional value chains with a view to achieving inclusive and sustainable economic growth).
Balozi Kayumba alisema, kupitia kaulimbiu hiyo, mengi yamefikiwa na cha muhimu zaidi eneo la SADC limeendelea kuwa salama na tulivu na kuongeza kuwa, “hatujashuhudia kuibuka kwa migogoro mipya, migoro mikubwa ya matumizi ya silaha au matendo ya ugaidi katika nchi wanachama tofauti na ile ambayo imekuwepo tokea zamani.”
Mkutano huo utakaofanyika takribani kwa siku 10, umegawayika katika makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkutano wa Kamati ya Fedha Agosti 10, 2023, Mkutano wa Baraza la Mawaziri Agosti 13 na 14 2023, Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ushirikiano wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama Agosti 16, 2023 na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC 17 Agosti 17, 2023.
Masuala mbalimbali yenye lengo la kuleta ustawi wa jamii, kuimarisha uchumi na usalama katika Kanda ya SADC yatajadiliwa katika ngazi tofauti za Mkutano huo, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya pamoja ambayo imeainishwa katika Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda, utekelezaji wa Bajeti na hali ya michango ya nchi wanachama na Maendeleo ya Viwanda na Mtangamano wa Masoko.