Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Qassem Soleimani amemshukia Rais wa Marekani, Donald Trump akionya kuwa jeshi lake litaivuruga nchi hiyo.
Mkuu huyo wa Majeshi amekaririwa na shirika la habari la Iran la Tasnim akimtahadharisha Trump kuwa kama Marekani itaanzisha vita basi jeshi lake litaimaliza kwa kuharibu kila kitu.
Jenerali huyo amesema kuwa ameamua kumjibu Trump kwani yeye ndiye anayehusika zaidi na masuala ya kijeshi; na kwamba ni kumsumbua rais wa nchi hiyo kujibu vitisho vya Marekani.
“Ongea na mimi sio na rais wetu [Hassan Rouhani]. Sio heshima kwa rais wetu kukujibu wewe,” amesema Meja Jenerali Qassem akijibu kauli ya Trump aliyoitoa hivi karibuni kupitia Twitter akiionya Iran kutojaribu kuitishia Marekani kwani itahabiwa kama ilivyokuwa kwa wababe wa nchi nyingine katika historia.
“Tuko karibu na wewe, ambapo hata huwezi kupata picha. Njoo. Tuko tayari. Ukianzisha vita, sisi tutaimaliza. Unajua kuwa hii vita itaharibu kila kitu unachomiliki,” alisema Mkuu huyo wa Majeshi ya Iran akimlenga Trump.
Kauli hizo zimeibuka baada ya Trump kuvunja makubaliano ya silaha za nyuklia ya mwaka 2015 kati ya nchi hizo (nuclear deal).
Lakini pia hivi karibuni Rais wa Iran aliitahadharisha Marekani kuwa isijaribu kuanzisha vita kwani kuanzisha vita na nchi hiyo ni sawa na kuanzisha vita mama na dunia nzima.
Trump alijibu kupitia Twitter akiweka msisitizo wa maandishi ya herufi kubwa akiitaka kutojaribu kuitishia Marekani tena.
To Iranian President Rouhani: NEVER, EVER THREATEN THE UNITED STATES AGAIN OR YOU WILL SUFFER CONSEQUENCES THE LIKES OF WHICH FEW THROUGHOUT HISTORY HAVE EVER SUFFERED BEFORE. WE ARE NO LONGER A COUNTRY THAT WILL STAND FOR YOUR DEMENTED WORDS OF VIOLENCE & DEATH. BE CAUTIOUS!
— Donald J. Trump (@realDonaldTrump) July 23, 2018
Iran na Marekani wamekuwa katika mgogoro wa muda mrefu. Hivi sasa nchi hizo zinakwaruzana pia kwenye mgogoro wa Syria, ambapo Iran inasaidia majeshi ya Serikali ya nchi hiyo ikiwa pamoja na Urusi huku Marekani ikisaidia upande wa wapinzani wao.