Mkuu wa Jeshi la Niger, jenerali Ahmed Mohamed amefukuzwa kazi zikiwa zimepita siku tano tangu wanamgambo wa kigaidi kuwaua wanajeshi 89 walipovamia kambi ya jeshi la Niger, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya wanajeshi kuuawa kwa siku moja.

Mbali na jenerali Mohamed, viongozi wengine waandamizi watatu wa jeshi hilo wamevuliwa nyadhifa zao katika uamuzi uliotangazwa na kituo cha habari cha taifa hilo baada ya kikao cha baraza la mawaziri.

Uamuzi huo umekuja wakati Rais wa nchi hiyo, Mahamadou Issoufou akiwa nchini Ufaransa pamoja na viongozi wa mataifa mengine ya Afrika Magharibi yanayosumbuliwa na ugaidi (Chad, Mali, Burkina Faso na Mauritania).

Viongozi hao wamekutana na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kujadili mikakati ya kijeshi kukomesha ugaidi katika ukanda wa Sahel.

Kwa kipindi cha miaka miwili ambacho jenerali Mohamed ameongoza jeshi kumekuwapo na ongezeko la mashambulio yanayotekelezwa na kundi la Kiislamu lenya mfungamano na al-Qaeda na kundi la Dola ya Kiislamu (IS).

Nafasi yake imechukuliwa na Meja Jenerali Salifou Modi, huku taifa hilo likitangaza siku tatu za maombolezo kutokana na vifo hivyo vilivyotokea katika kambi ya Chinegodar mkoani Tillaberi.

Mwezi uliopita jumla ya wanajeshi 71 waliuawa katika Kambi ya Inates mkoani humo.

TRA yatuma salamu za shukrani kwa walipakodi baada ya kuvunja rekodi
Kenyatta apangua safu ya Mawaziri

Comments

comments