Mkuu wa mkoa Mbeya, Albert Chalamila amewacharaza bakora wanafunzi 14 wa shule ya Sekondari Kiwanja iliyopo mkoani kwake katika wilaya ya Chunya kwa kosa la kumiliki simu shuleni  kinyume na sheria.

Wanafunzi hao wanahusishwa na tukio la kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo ambayo yaliteketezwa Oktoba mosi 2019 wakitaka kulipiza kisasi mara baada ya kunyang’anywa simu huku wanafunzi wengine watano wakishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.

Mkuu wa shule hiyo, Elly Mnyarape amesema Septemba 30, 2019 mchana walifanya msako na kukamata simu 26, na usiku wake mabweni hayo yaliteketezwa kwa moto.

Chalamila alichukua uamuzi huo mara baada ya kutembelea shule hiyo na kupokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa shule kuwa baadhi ya wanafunzi wanamiliki simu kinyume na sheria.

Baada ya kumaliza kuwapa adhabu Chalamila amemtaka Mkuu wa Shule kuwachukulia hatua za kinidhamu wanafunzi hao ili iwe fundisho kwa wanafunzi wengine waliopo shuleni hapo.

Lakini pia ameliagiza jeshi la polisi kuhakikisha wazazi wa watoto hao waliokutwa na simu kila mmoja analipa shilingi milioni moja zitakazotumika kukarabati mabweni hayo yaliyoteketezwa.

Aidha, katika mitandao ya kijamii imesambaa video ikimuonesha Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila akiwa na fimbo mbili moja akiwa ameshikilia mkono wa kushoto na nyingine mkono wa kulia akiwachapa fimbo tatu tatu wanafunzi hao kwa utomvu wa nidhamu na kuvunja sheria za shuleni hapo.

Lissu asaini mkataba na kampuni ya kimataifa kumsimamia kisheria
Polisi yajipanga kuimaliza Yanga, yaanza na motisha