Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ameagiza kuundwa kamati maalumu ya uchunguzi itakayopitia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa mkoani humo kutokana na taarifa za ufujaji wa shilingi bilioni 3.9.

Akizungumza kwenye Kikao cha Ushauri cha Mkoa huo (RCC), Gabriel ameitaka kamati itakayoundwa ianze na uchunguzi wa fedha za miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa fedha zinazotolewa na Serikali.

Amesema ubadhirifu umeanza kuonekana kwa Shule ya Msingi Kalemani ambayo ilipewa Sh 66 milioni, Sh 60 milioni kwa ajili ya vyumba vya madarasa na Sh 6 milioni kwa kujenga choo, lakini fedha zote zimetumika kujenga madarasa matatu ambayo hayajakamilika.

Sambamba na hayo pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na vyombo vingine vya kisheria kuchunguza ili fedha zote zilizofujwa zirejeshwe na kutaka idara ya ukaguzi wa ndani ya halmashauri kuchunguzwa juu ya utendaji wao.

Februari 17, 2020 Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato liliwasimamisha watumishi 15 wakiwemo sita wa idara ya manunuzi wakituhumiwa kufanya ubadhirifu wa Sh 3.9 bilioni za miradi ya maendeleo.

Weusi waandika barua vifo vya Viongozi
Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha afariki