Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar, Ayoub Mohamed Mahmoud (pichani) amewataka waananchi kusherehekea sikukuu ya Eid El Hajj, Septemba Mosi, kwa amani na kuzingatia sheria kwani Serikali ya Mkoa huo itaimarisha ulinzi na kuwachukulia hatua kali watakaojihusha na uhalifu.

Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo leo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari. Amesema Serikali ya mkoa huo itaendesha oparesheni maalum ya usalama, kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto na kuwachukulia hatua kali madereva wazembe.

“Tunawaomba watumiaji wa vyombo hivyo (vya moto) kuhakikisha kuwa vyombo vyao vimekaguliwa na mamlaka husika za ukaguzi na kupatiwa ruhusa ya kukubalika kwa vyombo hivyo kutumika barabarani kisheria ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni ya njia(road licence) pamoja na bima (insurance),” ameeleza kupitia taarifa hiyo.

“Hivyo, kwa taarifa hii, Mkoa unaagiza kuwa wale wote ambao vyombo vyao havijapasishwa na mamlaka husika, wasiviingize vyombo hivyo barabarani kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi na kusababisha ajali zinazoweza kuepukika,” ameongeza.

Mahmoud amesema kuwa jumla ya viwanja vya sikukuu 29 katika wilaya zote tatu za mkoa huo vitatumika katika kusherehekea sikukuu hiyo ya Eid El Hajj kuanzia majira ya alasiri na kwamba muda wa kufunga utatofautiana kulingana na mazingira ya kiwanja husika.

Aidha, Mkuu huyo wa MKoa wa Mjini Magharibi amesema kuwa ni marufuku kupiga muziki kwenye viwanja vyote vya sikukuu. Kwa upande wa vilabu na kumbi za starehe, amesema wataendelea kufuata utaratibu wa muda uliopangwa na Serikali ya mkoa huo kwa kupiga muziki kuanzia saa 2:30 usiku na kuhakikisha hawavuki saa 6 kamili usiku.

Kuhusu uuzwaji wa vyakula, amesisitiza kuwa watakaoruhusiwa kuuza vyakula katika viwanja vya sikuu ni wale tu ambao wamefuata taratibu za kupata vibali katika mabaraza ya manispaa na kuthibitishwa akiwataka pia kuzingatia usafi.

Waumini wa dini ya Kiislam watasherehekea Sikukuu ya Eid El Hajj, Septemba Mosi mwaka huu.

 

Magazeti ya Tanzania leo Agosti 31, 2017
Video: DC Mjema ateta na wadau wa maji jijini Dar