Mkuu wa Wilaya ya Makete mkoani Njombe, Veronica Kessy amesema kuwa wilaya hiyo imemaliza zoezi la kugawa Vitambulisho vyote 6,000 vilivyotolewa na Rais, Dkt, John Pombe Magufuli kwaajili ya Wafanyabiashara wadogo wadogo wilayani humo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la umoja wa Wanawake wa chama cha mapinduzi UWT Wilaya ya Makete, ambapo amesema kuwa Wajasiriamali ambao wamepewa Vitambulisho hivyo ni wale ambao mitaji yao haizidi milioni nne kwa mwaka.
Amesema kuwa kupitia Vitambulisho hivyo 6,000 Wilaya ya Makete imefanikiwa kukusanya na kuingizia Serikali fedha za Kitanzania kiasi cha shilingi Milioni 120 na kuiwezesha Wilaya hiyo kushika nafasi ya kwanza kati ya Wilaya nne za mkoa wa Njombe katika zoezi hilo la utoaji Vitambulisho.
“Wilaya yetu ya Makete tumefanikiwa kukamilisha zoezi la ugawaji vitambulisho vya Wajasiriamali, tulikuwa na vitambulisho 6,000 hadi nazungumza nanyi hapa Vitambulisho vyote vimeisha nasema tuko salama,”amesema DC Kessy
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Makete amesema kuwa awali baadhi ya Wananchi walikuwa na mashaka juu ya uendeshaji wa zoezi hilo lakini Serikali ilitoa elimu ya kutosha kwa Wajasiriamali wilayani humo na kufanikiwa kumaliza Vitambulisho vyote bila matatizo.
Kwa upande wao, Wabunge wa Viti Maalumu mkoa wa Njombe kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Dkt, Susan Kolimba na Neema Mgaya, walishiriki kikao hicho ambao kwa pamoja wameipongeza Serikali wilayani Makete kwa utendaji wake mzuri na kutatua matatizo ya Wananchi.