Aliyekuwa Mchezaji na Kocha Mkuu wa Young Africans Charles Boniface Mkwasa ameuangalia ubora wa timu yake hiyo ya zamani na ule wa Simba SC na kutoa tathimini ya mchezo wa kesho Jumapili (April 16).
Miamba hiyo itakutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kuanzia saa kumi na moja jioni, huku kila upande ukiwa na matumaini mazito ya kuibuka na ushindi utakaowapa alama tatu muhimu.
Licha ya kuwataja Clatous Chama na Fiston Mayele katika mchezo huo, Mkwasa amesema ubora wa Simba SC unakuwa zaidi kwa washambuliaji, wakati Young Africans itatawala kwenye beki katika mechi hiyo.
“Japo mara nyingi dabi hizi huwa na ufundi mdogo, kwa kuwa kuna kukamiana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki, ila ni mechi ngumu na kila upande una nafasi ya kufanya vizuri.
“Kitakachoamua matokeo ni namna kila timu itakavyojipanga, mikakati ya kila timu na namna kila moja itakavyofanikiwa kuzuia, kukaba na wepesi wa wachezaji.
“Timu zote mbili zina wachezaji wazuri, wako ‘dynamic’ (wana nguvu) kwa Young Africans Mayele ukimuachia kidogo tu anakufunga, Simba SC kina Chama wanaweza kutengeneza mipango ya ushindi.
“Hapo ni namna ya kuthibitiana, timu itakayozubaa inafungwa, ingawa ukiangalia Simba wana wachezaji wazuri mbele, wenye uwezo wa kufunga na hawana mtu maalumu wa kufunga, yeyote anaweza kufunga.
“Udhaifu wao upo kwenye beki hasa katika ukabaji, kocha anapaswa kufanya kazi ya ziada kwenye hilo kwani kuna watu wanaonekana hawana wepesi wa kuona makosa na kurekebisha kwa haraka,” amesema Mkwasa.
Amesema Young Africans ina viungo wazuri, japo kwenye kufunga, inamtegemea zaidi mtu mmoja, ambaye kama atadhibitiwa itakuwa ni kazi ya ziada.
“Ukiangalia wafungaji, Young Africans anaongoza Mayele (mabao 16), anayemfuatia kuna pengo kubwa (hadi kwa Aziz Ki mabao nane), wakati Simba SC ni Moses Phiri (10), John Bocco (9), Pape Ousmane Sakho na Jean Baleke (7),” amesema