Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Charles Boniface Mkwasa, amesema haikuwa rahisi kwa kikosi chake kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhiudi ya Chad, kutokana na umahiri wa wapinzani wao.

Mkwasa ambaye jana alikishuhudia kikosi chake kikiongozwa kwa mara ya kwanza na nahodha Mbwana Samatta, amesema Chad, walikua na uwezo mkubwa wa kupambana wakati wote, lakini alijitahidi kuwahimiza wachezaji wa Stars wafanye bidii ya kukamilisha kazi ya kusaka ushindi.

Mkwasa ameongeza kwamba mbali na upinzani mkali, pia kikosi chake kililazimika kucheza katika hali ya hewa ya joto kali, lakini pia kilifanikiwa kushindana na hali hiyo mpaka kikamaliza dakika 90 kwa kuziweka kibindoni point tatu muhimu.

“Hali ya hewa ilikuwa mbaya kabisa lakini vijana wangu walijituma na wanastahili pongezi kabisa,” alisema.

“Kipindi cha pili walitushambulia sana, lakini ilikuwa ni lazima kufanya hivyo ili kuhakikisha tunajilinda kuhakikisha hawasawazishi.”

Bao la Stars, katika mchezo huo, lilifungwa na Mbwana Samatta, katika kipindi cha kwanza.

Stars sasa imefikisha pointi 4 baada ya kucheza michezo mitatu, ikiwa imepoteza mchezo mmoja dhidi ya Misri, sare moja dhidi ya Nigeria na kushinda mmoja dhidi ya Chad.

Hata hivyo, Stars inaendelea kubaki katika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi H, ikitanguliwa na Nigeria yenye point 4 kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Misri ikiongoza kwa kufikisha point 6 na Chad wanaburuza mkia.

Licha Ya Marekebisho Ya Ratiba Ya VPL Manara Aikumbusha Tena TFF
Afungwa Maisha Jela kwa Kunajisi