Mlainda Lango wa Azam FC Ali Ahamada amewatupia lawama Mashabiki wa Soka la Bongo, kwa kusema hawana uvumilivu hasa timu inapopoteza ama kupata sare.
Ahamada raia wa visiwa vya Comoro, amefunguka hilo kufuatia kutupiwa maneno ya lawama na Mashabiki ambao walionesha Kuchukizwa na kiwango chake wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mabingwa Watetezi Young Africans.
Miamba hiyo ya Dar es salaam ilikutana Desemba 25 kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 19 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Azam FC ilikubali kupoteza 3-2.
Ahamada amesema kutokana na hali hiyo, hana budi kuzoea mazingira ya Soka la Bongo, ambayo amekiri yana tofauti kubwa na sehemu nyingine alizowahi kucheza Soka lake.
Hata hivyo Mlinda Lango huyo anayedaiwa kuwa mchezaji anaepokea Mshahara mkubwa nchini Tanzania, amesisitiza kuwa bado anatambua ana ubora wa kukaa langoni na atadhihirisha hilo kwa vitendo.
“Ni mapema sana kutoaminiwa ndani ya timu kwa sababu ni mara ya kwanza kucheza soka Afrika, Nafurahi kucheza soka la Tanzania,”
“Nimegundua ni nchi ambayo mashabiki wake wanapenda mpira lakini siyo wavumilivu timu inapopata matokeo mabaya.”
“Ushindi dhidi ya Simba SC hapakuwa na pongezi kutoka kwa mashabiki, ila baada ya kufungwa na Young Africans ni siku ambayo niliuchukia mpira kwa sababu nilisikia maneno mengi na kubaini kuwa hii nchi haina uvumilivu kwenye matokeo.” amesema Ahmada
Hata hivyo tayari Azam FC imeshatangaza usajili wa Mlinda Lango mpya kutoka nchini Ghana Abdulai Iddrisu, ambaye anatarajiwa kumpa changamoto Ahamada kwenye kikosi cha kwanza klabuni hapo.
Abdulai Iddrisu amejiunga na Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Bechem United ya kwao Ghana.
Ahamada alihiunga na Azam FC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Klabu ya Santa Coloma ya Andorra.
Kabla ya hapo Mlinda Lango huyo mwenye umri wa miaka 31, aliwahi kucheza soka akiwa na Klabu ya Toulouse (2011–2016) ya Ufaransa, Kayserispor (2016–2018) ya Uturuki, Kongsvinger (2019–2020) na Brann (2020) ya zote za Norway.