Mlinda Lango wa Klabu ya Chelsea, Robert Sanchez ameiunga mkono timu yake kwa kusema itafuzu michuano ya Ligi Mabingwa Barani Ulaya baada ya kupata sare ya mabao 4-4 dhidi ya Manchester City, kwenye mechi ya Ligi Kuu England mwishoni mwa juma lililopita.
Chelsea ilianza vibaya imsimu huu lakini wamepata matumaini baada ya kiwango bora walichoonyesha dhidi ya timu ngumu Manchester City, pamoja na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Tottenham.
Baada ya Chelsea kuonyesha ahueni kwenye safu ya ushambuliaji Mlinda Lango Sanchez, anaiona Chelsea ikifanya vizuri na kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Alipoulizwa katika eneo ambalo limeimarika zaidi baada ya mechi ya Jumapili (Novemba 12) na kuhusu uwezekano wa Chelsea kutinga Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mhispania huyo alisema: “Ikiwa tutaendelea kuimarika kila mechi na kupata alama muhimu nadhani inawezekana. Ni swali kubwa. Lakini kama ninavyosema, tuna ari, ujasiri, imani na tunajua ubora tulionao, tunaweza kufika huko.”
Chelsea inayonolewa na Mauricio Pochettino bado ana kazi ya kufanya kuboresha kikosi chake baada ya kutumia pesa nyingi kwenye usajili.
Vijana wa Pochettino wako nafasi ya 10 ikizidiwa alama 10 kutoka timu iliyoko kwenye nafasi ya nne za juu. Ingawa uwezekano wa The Blues kupanda nafasi za juu zaidi ni mdogo kutokana na majeruhi wengi iliyonayo.
Chelsea inatakiwa ipambane kutinga nafasi nne za juu ingawa inaweza ikaangukia pia nafasi ya tano ambayo ina nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kutokana na kanuni mpya iliyoanzishwa.
Ligi Kuu England kwa sasa imesimama kupisha michuano ya kimataifa na ikirejea itakabiliana na mpinzani mwingine wa nafasi nne za juu watakaposafiri St Jarmes Park kumenyana na Newcastle United Novemba 25.