Mlinda Lango wa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ Benedict Haule amesema wapo tayari kuwakabili Mabingwa watetezi wa Tanzania Bara Simba SC katika mchezo wa Mzunguuko wa 14 utakaopigwa leo Alhamis (Februari 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC iliyokabiliwa na matokeo mabovu katika michezo mitatu ya Ligi Kuu iliyopita, itakua mwenyeji wa mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa soka nchini kote.

Haule amesema wamekamilisha maandalizi yao kuelekea mtanange huo, na wana matumaini mkubwa ya kupambana na kupata ushindi ugenini, licha ya kutopewa nafasi hiyo na wadau wengi wa soka kwa kisingizio cha udhaifu wa kuburuza mkia wa Ligi Kuu.

Amesema wanaifahamu Simba SC ni timu kubwa na hawana budi kuiheshimu, lakini kwa maandalizi walioyafanya watakua na muda mzuri wa kunyakua alama tatu muhimu ndani ya dakika 90 za mchezo huo.

“Tumejiandaa kikamilifu, tunaamini tuliofundishwa katika kipindi cha kujiandaa na mchezo huu tutayafanyia kazi ili kupata alama tatu ambazo zimetutoa nyumbani kuja hapa Dar es salaam, tunaifahamu vizuri Simba SC kuwa ni timu kubwa hapa nchini, lakini hatuna budi kupambana ili kutimiza lengo letu.”

“Sisi kama Tanzania Prisons tunaiheshimu sana Simba SC, licha ya watu wengi kwa sasa kuibeza kutokana na matokeo walioyapata siku za karibuni, lakini kwetu tunaamini bado ina kikosi kizuri na tutafanya makosa kama tutaingia kwenye mtego wa kumdharau mpinzani.”

Tanzania Prisons inakwenda kuikabili Simba SC ikiwa inaburuza mkia wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 11, huku wenyeji wao wakiwa nafasi ya pili kwa kufikisha alama 25.

Dembele amshangaza Rais FC Barcelona
Bumbuli: Ahemd Ally aendelee hivyo hivyo, ni mdogo sana