Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kutofanyia kazi maombi ya mbunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kwani ni mtego.
Akichangia bungeni jijini Dodoma, Mlinga alirejea ombi la mbunge wa Chadema kwa Rais Magufuli ikimsihi kuingilia kati suala la Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuendelea kusota rumande kwani ni mtego wa kuingilia uhuru wa mhimili wa Mahakama.
Mbowe na Matiko wako rumande baada ya Mahakama kuwafutia dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana yao.
“Mheshimiwa Mwenyekiti nataka nimwambie Rais wangu mimi bado ni kijana mdogo sana. Asije akaingia kwenye huu mtego hata wakimfuata kwa kuburuza magoti,” alisema Mlinga.
“Chadema ndio wamekuwa wakizunguka dunia nzima kusema Rais hafuati Katiba, hafuati sheria, hafuati kanuni za nchi hii… yeye ni dikteta,” aliongeza.
Aidha, Mlinga alizungumzia madai ya baadhi ya watu kuwa Tanzania hakuna uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari. Alikanusha madai hayo akitoa mfano wa jinsi ambavyo kuna idadi kubwa ya vyombo vya habari ukilinganisha na mataifa mengine, na kutumia mfano wa katuni za mchoraji maarufu, Masoud Kipanya kuonesha uwepo wa uhuru huo na kwamba yeye binafsi asingeuvumilia.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuthibitishiwa hilo, tuambiwe ni mwandishi gani wa habari ambaye sasa hivi yuko jela kama hakuna freedom of expression (uhuru wa kujieleza). Msheshimiwa mwenyekiti kuna mchora katuni mmoja anaitwa Masoud [Kipanya] kwa katuni anazomchora Mheshimiwa Rais ningekuwa mimi nisingemuacha,” alisema.
Mbunge huyo wa Ulanga alisisitiza kuwa mambo hayo ya ukosoaji kupitia vyombo vya habari yanafanyika na yamekuwa yakiachwa, lakini alionesha kushangazwa na kauli za madai kuwa hakuna huru wa kujieleza nchini.