Wakati Dirisha la Usajili likitarajiwa kufunguliwa baada ya msimu wa 2022/23 kufikia kikomo mapema mwezi ujao, Mlinda Lango wa Klabu ya Chambishi FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia, Ally Baruti ‘Casillas’ ameonesha nia ya kutaka kucheza Soka katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2023/24.
Mlinda Lango huyo amefunguka matamanio yake ya kuvuka mpaka na kuingia Tanzania kwa ajili ya kusakata kabumbu, huku akizitaja Simba SC na Young Africans ambazo zitaboresha vikosi vyao kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi na Michuano ya Kimataifa.
Kinda huyo mwenye asili ya Tanzania ambaye pia aliipandisha daraja kwenda Ligi Kuu ya Zambia, Real Nakonde huku akiwa amebeba tuzo kadhaa ikiwamo mchezaji bora wa mechi zaidi ya mara mbili, amesema japokuwa soka la Zambia lina ushindani mkubwa na maslahi mazuri lakini anapenda kucheza Tanzania ili kutoboa zaidi.
Baruti ambaye ni mwenyeji wa Tabora akiibuliwa na kituo cha Ifa na Igunga FC alicheza Kimondo ya Mbeya akiwa na miaka 15 na kuchukuliwa na Real Nakonde ya Zambia ikiwa daraja la kwanza na kuipandisha daraja akatimkia Tazara Rangers.
“Baada ya hapo nikajiunga na Jumulo FC ya Kitwe iliyokuwa inashiriki Nationa League kwa mkataba wa miaka miwili na nusu na sasa nacheza Ligi Kuu katika klabu ya Chambishi kwa mkopo wa mwaka mmoja,” amesema
Akizungumzia nia yake ya kucheza Soka katika ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena, Ally amesema; “Kuna viongozi wengi na mawakala wa huko Tanzania wameniambia nikifika timu ni nyingi na wana uwezo wa kunitafutia timu, soka la Zambia ni soka la usindani na Ligi Kuu ya huku ni nzuri inafuatiliwa na nchi nyingi za Afrika,” amesema