Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amewataka wanachama wa chama hicho waliotia nia ya kugombea ubunge lakini hawakuteuliwa kutobabaika na badala yake watulie kwa vile ana uhakika zipo kazi nyingine anazoweza kuwapatia.

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akiwasalimia wakazi wa Kata ya Tinde wilayani Shinyanga akiwa njiani kuelekea mjini Shinyanga akiendelea na kampeni za kuomba kura kutoka kwa wakazi wa mkoa.

Amewataka wanachama wa chama hicho kuheshimu maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

“Ndugu zangu tuache kulalamika, tukipiganie chama chetu kiweze kushinda katika nafasi zote tatu, udiwani, ubunge na urais, na hapa Solwa nileteeni Ahmed Salum, msinichanganyie na wale wa upinzani, hapa tunahitaji mtu wa CCM, hatuhitaji sura ya mtu, mkinichagua mimi ndiyo nitakuwa Rais,” amesema Magufuli.

“Nataka niwaambie ukweli, nikiwa rais mnafikiri nitaacha kumpa kazi Masele (Stephen), siwezi kumuacha hivi hivi. Ninawaeleza hivi kwa sababu sisi CCM tunafahamu, lakini pia maamuzi ya NEC lazima yaheshimike, kwamba tukimleta huyu atatuleta hapa, siyo Shinyanga tuwe tunashinda kwa kura moja, hapana,” ameeleza Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli ameendelea kunadi ilani ya chama chake akiwaomba wananchi wamchague ili awatumikie kwa muhula wa pili utakaokamilika mwaka 2025.

Tutaboresha sera na mifumo, sekta ya Madini -JPM
KITAELEWEKA: Messi kubaki ama kuondoka Barcelona?