Ripoti za wataalamu wa Afya, zimeeleza kuwa mlipuko wa homa ya Denge, na Kipindupindu uliosababishwa na ukosefu wa maji, umeua mamia ya watu Nchini Sudan, huku wakitoa onyo kwa mlipuko huo kuwa unaweza kusambaa zaidi na kutatiza mfumo wa afya ulio katika hali tete.
Ripoti hiyo ya Chama cha Madaktari wa Sudan, pia kimeonya kuwa hali ya afya katika Jimbo la Kusini Mashariki la Gedaref, kwenye mpaka na Ethiopia, imekuwa mbaya kwa kiwango kikubwa, huku maelfu ya watu wakiambukizwa homa ya Denge.
Hata hivyo, japo mji huo wa Gedaref haujapata athari za moja kwa moja za vita baina ya Jeshi la Sudan na vikosi vya akiba vya (RSF), bado eneo hilo limekumbwa na mgogoro kutoka kwa watu waliokosa makazi na huduma za kibinadamu, ambapo zaidi ya miezi mitano ya vita, asilimia 80 ya Hospitali hazifanyi kazi.
Sekta ya afya isiyo madhubuti nchini humo, ilikuwa na wakati mgumu kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kila mwaka inayo endana na msimu wa mvua, kuanzia mwezi Juni ikijumuisha na Malaria na Denge kabla ya mapigano hayo kuzuka hali ambayo sasa inaashiria uwepo wa maafa makubwa.