Aliyekua mshambuliaji mahiri wa klabu ya Young Africans Mohamed Hussein “Mmachinga” ameonyesha wasiwasi kuhusu mchezo wa mkondo wa pili wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho ambapo wawakilishi pekee wa Tanzania watacheza dhidi ya MC Alger mwishoni mwa juma hili nchini Algeria.
Mmachinga amezungumza na Dar24 na kueleza wasiwasi wake kuelekea mchezo huo, ambapo amesema Young Africans wana wakati mgumu wa kwenda ugenini kupambana, kutokana na uhalisia wa MC Alger aliouona walipocheza hapa nyumbani mwishoni mwa juma lililopita na kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Amesema Young Africans walikua na kila sababu ya kutengeneza mazingira ya kuufanya mchezo wa mkondo wa pili kuwa na hali ya kawaida kiushindani, lakini kwa kushindwa kutumia vyema nafasi za kufunga katika mchezo wa jumamosi, inawatengenezea mazingira magumu ya kwenda kulinda ushindi wao ugenini.
“Katika soka lolote linaweza kutokea, lakini kwangu mimi siamini kama waarabu watakubaki kupoteza wakiwa nyumbani kwao, tena kwa kuwa nyuma kwa bao moja ambalo walifungwa hapa Tanzania, timu yetu ilipaswa kutafuta ushindi wa mabao zaidi ya mawili ili kujiweka katika mazingira ya kwenda ugenini wakiwa wanajianiami.
“Ninakuhakikishia mchezo wa mkondo wa pili utakua mgumu sana kwa Young Africans, na kikubwa zaidi waarabu wamekua na mbinu chafu nje na ndani ya uwanja, tena wanapokua kwao, hivyo nina wasiwasi mkubwa na mchezo huu wa pili.” Alisema Mmachinga.
Young Africans wanatarajia kuanza safari ya kuelekea nchini Algeria wakati wowote kuanzia kesho, na endapo watahitaji kusonga mbele, itawalazimu kulinda ushindi wao wa bao moja kwa sifuri ama waendelee kusaka namna nyingine ambayo itawawezesha kushinda ugenini.
Bao pekee na la ushindi katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa jumamosi kwenye uwanja wa Taifa, lilifungwa na kiungo kutoka nchini Zimbabwe Thaban Scala Kamusoko katika dakika ya 61.