Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima ni uvunjaji wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo na amewataka wafugaji wafuge mifugo yao kulingana na ukubwa wa maeneo yao ya malisho huku akisema jamii hizo ziache kugombana kila siku bila faida.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya Nanjaru na Mkaranga vya Kata ya Nambilanje na kijiji cha Nankonjera kilichopo Kata ya Namichiga akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Amesema, “Kilimo ni maisha, kilimo ni biashara, kilimo ni fedha na vivyo hivyo ufugaji ni maisha, ufugaji ni biashara na ufugaji ni fedha hivyo kila mkulima alime kulingana na ukubwa wa eneo lake na mfugaji afuge mifugo kilingana na ukubwa wa eneo lake na malisho. Sisi sote ni Watanzania na tunataka utajiri. Wakulima na wafugaji waheshimiane kwani wote ni Watanzania.”

Akina mama wakijiviringisha chini kama ishara ya heshima kumpokea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema migogoro baina ya wakulima na wafugaji haina tija na Serikali haitaki kuiona ikiendelea na kwamba kati yao hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine, hivyo kila mmoja aweke mpango kazi ambao hautaathiri upande wowote.

Aidha, amewataka watendaji wa vijiji kabla hawajagawa maeneo kwa wafugaji wahakikishe idadi ya mifugo waliyonayo na washirikishe Serikali ya kijiji na wananchi. “Wafugaji badilikeni fugeni kisasa, msione fahari kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo mnashindwa kuihudumia. Fugeni mifugo michache ambayo mtaihudumia vizuri na kuiuza kwa gharama kubwa.”

Man Utd wapotezea ishu za mawakala
Kocha Gamondi aomba mechi ya kirafiki