Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema kuwa hatafuata nyayo za mtangulizi wake, Robert Mugabe katika ‘kuhodhi’ madaraka.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na vyombo vya habari vya Marekani, Mnangagwa amesema kuwa anapanga kumpa nafasi ya uongozi aliyekuwa mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi uliopita, Nelson Chamisa.
Gazeti la Daily News limeeleza kuwa Mnangagwa ambaye alienda Marekani kwa ajili ya kikao cha Umoja wa Mataifa, alisema kuwa hatakuwa na pingamizi katika kuachia madaraka, kwani hivi sasa katiba yao imetoa ukomo wa mihula miwili ya urais.
“Hivi sasa tuna ukomo wa mihula miwili tu ya urais. Nitaiheshimu na kuizingatia bila pingamizi lolote,” alisema. “Ni lazima uwape nafasi watu wako kuwa na viongozi wengine,” aliongeza.
Alisema kuwa Serikali yake inapanga kuanzisha nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni, na kumpa ofisi rasmi mpinzani wake, jambo ambalo halikuwahi kufanyika hapo awali.
Alifafanua kuwa kutokana na cheo hicho, Chamisa atakuwa anapokea mshahara wa Serikali pamoja na huduma nyingine kama ilivyo kwa viongozi wa Serikali.
Mnangagwa alishinda kwenye uchaguzi wa Julai 30 mwaka huu, lakini mpinzani wake ameendelea kueleza kuwa kura zilichakachuliwa na hivyo sio rais halali.
Hivi karibuni, wabunge wa upinzani walitoka bungeni wakati Mnangagwa analihutubia bunge, wakipaza sauti zao wakimuita ‘mwizi’.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa MDC, chama kinachoongozwa na Chamisa waliliambia Daily News kuwa endapo Chamisa atakubaliana na mpango wa cheo hicho kwao itakuwa kama kukubali kupokea rushwa kutoka kwa Mnangagwa.