Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amemtumbua makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe, Levi Nyagura kutokana na tuhuma za kumtunuku Grace Mugabe shahada ya Uzamivu (PhD), miaka minne iliyopita bila kuzingatia taratibu.
Levi Nyagura, anakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi na kuvunja taratibu za Chuo Kikuu cha Zimbabwe kuhusu namna ya kutunuku PhD.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mnangagwa ambaye sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe, alisema kuwa nafasi ya Nyagura inachukuliwa na msomi mwingine, Paul Mapfumo ambaye atakaimu nafasi hiyo hadi kesi dhidi a Nyagura itakapomalizika.
Imeeleza kuwa kitendo cha kumsimamisha Nyagura kinatokana na taratibu na sheria iliyoanzisha Chuo Kiku cha Zimbabwe.
Grace ambaye ni mke wa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe anadaiwa kutofanya utafiti wake mwenyewe na kwamba alitumia muda mfupi zaidi kukamilisha masomo ya PhD tofauti na taratibu, hivyo inaonekana kuwa ilikuwa ni PhD feki.
Kwa mujibu wa tuhuma hizo zilizoibuka muda mfupi baada ya Mugabe kulazimika kujiuzulu nafasi yake ya urais, PhD hiyo ilitolewa kwa kumpendelea kwakuwa alikuwa mke wa Rais.
Grace alikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa yeye alifanya utafiti wake mwenyewe na kutoa baadhi ya mambo aliyoyafanya wakati alipokuwa anakusanya taarifa (data) kwa ajili ya kukamilisha utafiti huo ambao ni hitaji muhimu katika kuhitimu.
Awali, ilikuwa imedaiwa kuwa hakufanya kabisa utafiti huo, lakini Chuo Kikuu Cha Zimbabwe kilijibu kwa kuweka kwenye mtandao nakala ya utafiti wa Grace. Ikabaki suala la muda wa kufanya masomo na kuhitimu.