Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amemuomba Rais wa Urusi, Vladimir Putin kumsaidia kulikomboa taifa lake dhidi ya anguka la kiuchumi linaloikabili hivi sasa.
Akimuita Putin kama ‘kaka yake mkubwa’, Mnangagwa amesema kuwa Zimbabwe inamtegemea kiongozi huyo wa Urusi kusaidia kuwapa muongozo utakaotatua changamoto ya kiuchumi inayowakabili.
“Mheshimiwa Rais, ninategemea kwamba nchi zetu zinaingia katika ushirikiano, na nchi yetu ni nchi inayoendelea, ni nchi ya dunia ya tatu, hivyo wewe, kama kaka yangu mkubwa, unaweza kunishika mkono kwa namna ninavyojaribu kuiendeleza Zimbabwe,” amesema Mnangagwa.
Rais huyo wa Zimbabwe hivi sasa anafanya ziara katika nchi za Ulaya Mashariki na ratiba yake itaishia kwenye Kongamano la Dunia la Uchumi litakalofanyika mwezi huu mjini Davos nchini Uswizi.
Jana, alikutana na Rais Putin jijini Moscow na kufanya mazungumzo ambayo Ikulu ya Urusi ilieleza kuwa yalilenga katika kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo.
Hatua hiyo ya Rais Mnangagwa inakuja wakati ambapo kumekuwa na changamoto kubwa ya kiuchumi nchini kwake, huku mamia ya watu wakiingia barabarani kupinga kupanda kwa gharama za maisha ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta kwa 150%.
Hali ya utulivu imerejea leo katika mitaa ya jiji la Harare kufuatia siku tatu za mgomo wa kufanya kazi na maandamano ya kuishinikiza Serikali kuchukua hatua kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
Hali ya kukosekana kwa ajira nchini humo pia ni changamoto kubwa ikirekodiwa kufikia 80%.
Rais wa Zimbabwe amewaandikia pia ujumbe wananchi wake akiwataka kuwa watulivu na kutofanya vurugu wakati wa maandamano, akiwahakikishia kuwa anafanya jitihada za kuhakikisha wawekezaji zaidi wanaingia nchini humo hivi karibuni.