Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amekatisha ziara yake nchi za nje kufuatia kuongezeka kwa vurugu zilizosababishwa na vyombo vya ulinzi vinavyopambana na waandamanaji wanaoipinga serikali.
Kiongozi huyo alipaswa kuelekea jijini Davos, Uswisi kushiriki katika Jukwaa la Kiuchumi duniani, kwa lengo la kutafuta vitega uchumi kwa ajili ya kuinusuru nchi yake iliyoporomoka kiuchumi ambapo amesema kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni kuifanya Zimbabwe kuwa na utulivu na imara.
Maandamano hayo yamesababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta mwishoni mwa wiki iliyopita, huku kundi moja la haki za binadamu likisema majeshi ya ulinzi toka kuanza kwa maandamano hayo yameua watu kumi na mbili na kuwakamata zaidi ya mia moja.
Akizungumza na gazeti la serikali Msemaji wa Rais, George Charamba amekilaumu chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) kwa ghasia hizo zinazotokea kwa kuunga mkono waandamanaji.
”Kiongozi wa MDC imekuwa ikisisitiza ujumbe wake kwamba itatumia ghasia za mtaani kuyapindua matokeo ya uchaguzi wa mwaka uliopita” amesema Charamba.
Aidha, upinzani nchini humo umepinga uamuzi wa mahakama uliotolewa mwaka jana mwezi wa Nane kuthibitisha kwamba Rais Mnangagwa amemshinda mgombea wa MDC, Nelson Chamisa.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Zimbabwe kuacha kile ilichokiita matumizi ya nguvu yanayofanywa na jeshi kwa kinachoelezwa kuwa utafutaji wa nyumba kwa nyumba na kwa kutumia silaha za moto.