Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Christine Mndeme amezindua mradi wa Maji katika kijiji cha Mhande, Kata ya Ngh’ong’hona ambao umefadhiliwa na Shirika shirika la wamishionari wa damu takatifu ya Yesu (CPPS) uliogharimu kiasi cha Sh.Milioni 35.

Mradi huo umetokana na maombi ya Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde kwa Shirika hilo kusaidia kutatua changamoto ya Maji katika kata hiyo  ya Ngh’ongh’ona ambayo wananchi wake wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo kubwa la upatikanaji maji safi na salama.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mndeme amelishukuru shirika hilo la CPPS kwa ufadhili wa mradi huo na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kuwa mstari wa mbele kutatua kero za wanachi wake hususani kero kubwa ya maji katika kata ya Ngh’ongh’ona.

“Mwili unahitaji maji unapotafuta maji mbali roho inasononeka hata muda wa kusali unaukosa, tunashukuru sana shirika hili lakini wananchi tuna wajibu wa kuutunza mradi huu ambao ni wa thamani kubwa sana,”amesema Mndeme

Hata hivyo ameongeza kuwa hatasita kuwachukulia hatua watu watakaoharibu miundombinu ya mradi huo wa maji huku akiwataka kuunda kamati ya maji ili kuendesha mradi huo.

Naye, Diwani wa Kata hiyo Philipo Nangu amesema wananchi hao wamekuwa wakipata adha kubwa ya maji na kulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma hiyo vijiji jirani jambo lilosababisha kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.

 

Polepole azipita kando hoja za Chadema kuhusu hali ya Uchumi
Putin awatimua wamarekani nchini Urusi