Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imesema kuwa afya ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla inazidi kuimarika akiendelea na matibabu.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, uongozi wa hospitali hiyo umesema kuwa madaktari wanaomtibu wameomba vyombo vya habari kumpa nafasi ya kupumzika.
“Madaktari wanaomtibu Dkt. Kigwangala wameomba vyombo vya habari kumpa nafasi ili aweze kupumzika. Atanzungumza na umma wa Watanzania afya yake itakapoimarika zaidi,” imeeleza.
Waziri Kigwangala aliumia baada ya kupata ajali ya gari katika kijiji cha Magugu mkoani Manyara, Jumamosi iliyopita.
Gari la umma alilokuwa anatumia katika safari hiyo ya kikazi, akitokea Arusha kuelekea Dodoma lilipinduka, ndani yake wakiwemo pia maafisa wa Serikali na waandishi wa habari.
Ajali hiyo ilichukua uhai wa Afisa Habari wa Wizara hiyo, Hamza Temba. Mungu amrehemu.